Jinsi ya kuzitumia Shuhuda kwa haki


Je Ellen White alifundisha nini kuhusu namna ya kutumia maandiko yake? Watu wengi leo hunukuu sehemu fulani kutoka kwenye shuhuda ili kutetea kitu fulani ambacho Ellen White mwenyewe hakuwahi kukifundisha, jinsi hii ni kuyatumia maandiko yake katika njia isiyo haki. Hivyo tuangalie misingi ambayo Ellen White mwenyewe aliagiza ifuatwe wakati watu wanapotumia maandiko yake.

Msingi 1: Hakuna Andiko Lolote La Shuhuda Linalopaswa Kudharauriwa.

"Kuhusu Shuhuda hizi, hakuna kitu cha kudharau; hakuna kitu cha kuwekwa pembeni; lakini muda na mahali lazima vizingatiwe. Hakuna kitu cha kufanya bila kuzingatia muda. Baadhi ya mambo yanaweza kuondolewa kwa sababu baadhi ya watu watafanya matumizi yasiyo sawa katika nuru iliyotolewa. Kila nukta na joti ni vya lazima, na ni lazima vionekane katika muda unaofaa. Katika siku za nyuma, shuhuda ziliandaliwa kwa uangalifu kabla hazijatumwa kwenda kuchapishwa. Na vitu vyote bado vinasomeka kwa makini kama maandiko ya kwanza." —(Ellen G. White, Sellected Messages Book 1, p. 57, par. 2); pia The Writing and Sending Out of the Testimonies to the Church, p. 25a .1; The Paulson Collection of Ellen G. White Letters, p. 9.4; Manuscript 23, 1911 (October 10, 1911) par. 1)))

Katika Msingi huu tuna vitu vya kuangalia kwa makini, na kujua nini tumekatazwa kufanya na nini lazima tufanye wakati wa kuzitumia Shuhuda za Bwana. Ellen White anafundisha kwamba:

a. "hakuna hata nukta moja tu ya maandiko yake inayopaswa kudharauriwa." Hili ni tatizo kwa watafsiri wa vitabu vyake kutoka kingereza kuja kiswahili; kwa maana wanatafsiri sehemu flani tu ya kitabu na nyingine wanaiacha, kuna vitabu vingi vya namna hiyo lakini nitatolea mfano mmoja tu wa kitabu cha "Pambano Kuu" ambacho kina kurasa 331 tu; wakati kimetafsiliwa kutoka katika kitabu cha kiingereza cha "The Great Controversy" ambacho kina kurasa kama 694. Watafsiri wanakiri kwamba walikifupisha kitabu hicho. Lakini pia hii ni onyo kwa watu wote ambao hudharau baadhi ya maneno ya kwenye Shuhuda kwa sababu yanawafunua kwamba wako kwenye kosa, na huwa wanayatumia badhi tu ya maneno ya Shuhuda ambayo yanaonekana kuwaunga mkono au yanawatetea upande flani. Hakuna neno lolote la Ushuhuda la kupuuzia.

b. "hakuna kitu cha kuwekwa pembeni". Yaan, hakuna kitu cha kuacha na kusema kwamba 'tutafsiri hiki ni cha muhimu na tusitafsiri hiki sio cha muhimu kwenye kitabu hiki', hakuna kitu cha kuweka pembeni na kusema hakina umuhimu. Kuna baadhi ya watu ambao Shuhuda zinapoonyesha kwamba wako kwenye kosa lililo wazi, badala ya kumshukuru Mungu kwa kuwaonyesha kosa lao, wao "wanaweka pembeni" sehemu flani ya ushuhuda ili wawe huru kuendelea katika kosa. Hii ndiyo njia ambayo shetani anataka watu waipitie kuelekea uharibifu; maana anajua kabisa kwamba "pasipo maono watu hupotea" Mithali

c. "muda na mahali lazima vizingatiwe, hakuna kitu cha kufanya bila kuzingatia muda". Kuna Shuhuda ambazo hazihitaji kuzingatia muda wala mahali, lakini pia kuna shuhuda nyingine muda na mahali jambo lilipotokea lazima vizingatiwe ili Shuhuda zisitumike kutetea kosa. Hauwezi kutumia ushuhuda wa mwaka 1893 kutetea kanisa la mwaka 2017 labda tu kama limeendelea na hali ileile, vivyo hivyo huwezi kutumia ushuhuda wa mwaka 1893 kulikemea kanisa la mwaka 2017 labda tu kama limeendelea katika hali ileile. Muda na mahali ambapo jambo flani lilitokea ni lazima vizingatiwe katika kutumia Shuhuda, bila hivyo Shuhuda zitatumiwa nje na maana zake halisi.

d. "kila nukta na joti ni vya lazima, na ni lazima vionekane katika muda unaofaa". Hii ndio njia halali ya kutumia shuhuda, sio njia ya kuweka pembeni baadhi ya maneno, bali ni kutumia joti zote kwa kuzingatia muda mwafaka.

Msingi 2: Shuhuda Zinajifafanua Zenyewe.

"Kuna wale ambao watatafisiri vibaya jumbe ambazo Mungu amezitoa, kulingana na upofu wao wa kiroho. . . .Shuhuda zenyewe zitakuwa ufunguo ambao utaelezea jumbe zilizotolewa, kama Maandiko yanavyoelezewa kwa Maandiko." —(Ellen G. White, Letter 73, April 24, 1903, par. 7); pia Selected Messages Book 1, p. 41.5; Ye Shall Receive Power, p. 252.5; Believe His Prophets, p. 207.3)))

Msingi huu ni msingi muhimu sana katika kutumia maandiko ya Ellen White, hakuna mtu anayepaswa kutafsiri kwamba hiki kinamaanisha hivi, na hiki kinamaanisha hivi. Lakini Shuhuda zote zinapaswa kukusanywa kwa makini na kulinganishwa ili kupata uwiano wa haki, shuhuda zinapaswa kujifafanua zenyewe kwa zenyewe na kuleta uwiano wa haki na hukumu ya haki. Hii ndio njia ya haki ya kufafanua maandiko yoyote kwa kuyaacha yaongee menyewe kwa menyewe, lakini watu wameisukumia mbali njia hii na wanafuata utafsiri wa mwanadamu na kanuni za kibinadamu ambazo hazipatani na maandiko katika uwiano wa haki.

Msingi 3: Matumizi Ya Sehemu Flani Tu Ya Fungu, Na Kudharau Sehemu Nyingine Inayofuata.

". . . .najua watu wengi huchukua Shuhuda alizozitoa Bwana na kuzitumia kama wanavyodhani wangezitumia, wakichukua sentensi hapa na pale, wakiiondoa kutoka katika uhusiano wake sahihi, na kuitumia kulingana na mawazo yao. Hivyo roho dhaifu hudanganywa wakati, kama wangesoma katika utaratibu vyote ambavyo vimetolewa, wangeona matumizi ya kweli na wasingeweza kuchanganyikiwa. Vingi ambavyo vinaonekana kuwa ni ujumbe kutoka kwa Dada White, vinafanya dhumuni la kumwakilisha vibaya Dada White, na kumfanya yeye kushuhudia katika neema ya vitu ambavyo haviko katika mujibu wa mawazo yake au hukumu. Hii inafanya kazi yake kuwa ngumu sana." —(Ellen G. White, Manuscript 21, March 3, 1901, par. 11); pia Selected Messages Book 1, p. 44.3; Messenger of the Lord, p. 394.1; 530.8; The Voice of The Spirit, p. 110.5; na Basic Rules of Interpretation-Internal and External, p. 8.1)))

"Kwa nini watu hawataona na kuuishi ukweli? Wengi hujifunza Maandiko kwa lengo la kuthibitisha mawazo yao wenyewe kuwa sahihi. Wanabadilisha maana ya Neno la Mungu ili kupatanisha na maoni yao wenyewe. Na hivyo wanafanya pia kwa shuhuda anazotuma. Wananukuu nusu ya sentensi, na kuiacha nusu nyingine ambayo, kama ingenukuliwa, ingeonyesha hoja zao kuwa ni uongo. Mungu ana pambano na wale ambao hufanyia bidii Maandiko, na kuyafanya yaendane na mawazo yao ya zamani." —(Ellen G. White, Manuscript (Ms) 22, January 29, 1890, par. 16); pia Sellected Message Book 3, p. 82.3)

Kunukuu sehemu flani tu ya shuhuda sio vibaya kama sehemu hiyo ndivyo mwandishi alivyomaanisha, lakini kunukuu sehemu moja ya fungu ambayo mwandishi alikuwa bado anaendelea kuitolea maana sahihi, na kuiacha sehemu ya chini ambayo kama ingejumuishwa ndiyo ingeonyesha maana sahihi ya fungu hilo na hukumu sahihi ya mwandishi wake, hii ni kutumia vibaya na kupotosha hukumu; kwani msomaji ataamini maana ambayo ni ya uogo tofauti na maana halisi aliyoiaminisha mwandishi. Kuna vitabu vingi ambavyo wamenukuu sehemu moja na kuiacha nyingine ambayo kama wangeijumuisha ingefunua wazi wazo wanalolitetea kuwa ni uongo, na hivyo wakaishia kunukuu sehemu hiyo moja tu ili kutetea wazo lao ambalo haliko sahihi. Mfano wa vitabu hivyo ni kitabu cha Robert W. Olson cha "Dhiki Kuu Inakuja" (A Crisis Ahead), na kitabu cha kanisa cha "Matukio ya Siku za Mwisho" (Last Days Events); ni vitabu ambavyo kuna baadhi ya sehemu waandishi wake wamenukuu nusu ya fungu ili kutetea kitu flani, lakini kama ukiangalia nusu nyingine ya pili ambayo hawajaiweka hapo utaona kuwa Ellen White hakumaanisha kile wanachokifundisha. Kwa sasa sitaonyesha kwamba ni wapi na wapi makosa hayo yanaonekana katika vitabu hivyo, lakini hivi karibuni nitafanya hivyo na kuweka hapa ushahidi, au kiungo cha kuelekeza kwenye ushahidi. Hata hivyo, Ellen White anaendelea kulaumu juu matumizi ya "nusu fungu" kama hayo:

"Kuna baadhi ya waumini wanaodai kukubali sehemu fulani ya shuhuda kama ujumbe wa Mungu, wakati wanazikataa sehemu hizo nyingine ambazo zinalaani tamaa zao wanazopendelea. Watu kama hao wanafanya kazi kinyume na ustawi wao wenyewe, na ustawi wa kanisa. Ni muhimu kwamba tuenende katika nuru wakati tuna nuru." —(Ellen G. White, Manuscript (Ms) 71, June 18, 1908, par. 3); pia Sellected Message Book 3, p. 80, par. 5; Christian Leadership, p. 75.3; Counsels for the Church, p. 233.7; Counsels on Diet and Foods, p. 37.1; Counsels on Health, p. 128.1; na Ms 37, 1909, par. 7)))

"Inanivunja moyo kwao kuchukua sehemu katika ushuhuda ambazo zinawapendeza, ambazo wanazielezea kuhalalisha mwenendo wao wenyewe wa utekelezaji na kutoa hisia kwamba sehemu hiyo ambayo wao wanaikubali ni sauti ya Mungu, na kisha wakati Shuhuda nyingine zinapokuja ambazo zinaleta kemeo juu ya mwenendo wao, wakati maneno yaliyosemwa hayapatani na maoni yao na hukumu, wanaidharau kazi ya Mungu kwa kusema, "Oh, hii hatuwezi kukubali; ni maoni tu ya Dada White, na hayana ubora kuliko maoni yangu au mtu mwingine yeyote." Hii haimheshimu Mungu na ni ya kuhuzunisha kwa Roho wake." —(Ellen G. White, Letter (Lt) 3, January 25, 1889, par. 10); pia Sellected Message Book 3, p. 81.3; 1888 Materials, p. 254.1; na Manuscript Releases, vol. 5, p. 150.3)))

"Wakati ndugu zangu watumikao au washiriki wa kawaida wa kanisa, ili kutetea hatua, huchagua sentensi chache kutoka katika maneno niliyoyatamka au barua nilizoziandika, na kuzitumia sentensi hizi nje na uhusiano, hawanifanyii haki. Tafadhari mwacheni Dada White abebe ujumbe wake mwenyewe. Utakuja na neema bora kutoka kwake kuliko kutoka kwa mtu anayemtolea taarifa." —(Ellen G. White, Manuscript 21, March 3, 1901, par. 13)

Msingi 4: Haitakiwi Kutumia Vibaya Au Kutafsiri Vibaya Shuhuda.

"Nimelazimika kusema kwamba sidhani niko salama hata katika kuandika kwa ndugu zangu na lazima nikate chanzo hiki cha hatari, ili kwamba maneno yangu yasitumiwe vibaya. Sitaraajii nukta moja ya ushawishi wangu kutumiwa ili kujeruhi nafsi. Kwa maana ndugu zangu kukamata neno au maelekezo ambayo nimeyafanya, na kuyatafisiri kumaanisha kitu flani ambacho kamwe sijakimaanisha, inaumiza nafsi yangu vibaya sana. Jinsi gani wanadhani naweza kukamilisha kazi niliyopewa na Mungu wakati wanaingilia kati ya kazi ya Mungu ambayo amenipa mimi na nafsi nazopenda kuzisaidia. Ukimya ni ufasaha." —(Ellen G. White, Manuscript 21, March 3, 1901, par. 14)

"Kuna wengi ambao hutafsiri kile ninachokiandika katika nuru ya maoni yao wenyewe yasiyobadilika. Unajua hii inamaanisha nini. Mgawanyiko katika uelewa, na maoni yanayotofautiana ni matokeo ya hakika. Jinsi ya kuandika katika njia ya kueleweka kwa wale ambao nawashughulikia suala muhimu ni tatizo ambalo siwezi kulitatua. Lakini nitajitahidi kuandika kiasi kidogo. Kutokana na ushawishi wa akili juu ya akili, wale ambao hawaelewi wanaweza kusababisha wengine kutoelewa kwa ufafanuzi wanaoweka juu ya masomo kutoka katika kalamu yangu. Mmoja anayaelewa kama anavyodhani kuelewa, kwa mujibu wa mawazo yake. Mwingine anaweka ujenzi wake juu ya suala hilo lililoandikwa, na kuchanganyikiwa ndiyo matokeo ya hakika. Ninaogopa. Ninatetemeka kama ninavyofikiria kwamba mawazo ya ndugu zetu yasipokuwa chini ya udhibiti wa Roho Mtakatifu, hakika watasoma mambo haya katika nuru iliyopotoshwa." —(Ellen G. White, Letter (Lt) 96, June 21, 1899, par. 4); pia Sellected Message Book 3, p. 79.3&4; na Manuscript Releases, vol. 4, p. 56.2)))

Matumizi mabaya na kutafsiri vibaya maandiko ya Ellen White, inatokea kwa sababu ya kunukuu nusu tu ya fungu na kuiacha nusu nyingine ambayo ndiyo inaonyesha maana halisi. Hii huwaongoza watu kuamini kitu cha uongo huku wakidhani kwamba wanaamini ukweli kama ulivyoandikwa na dada White, huwaongoza watu kuzisoma Shuhuda katika nuru ya uongo na ya kudanganya. Lakini kama wangeangalia kifungu chote cha maneno wangepata maana sahihi, wala kuchanganyikiwa kusingekuwepo, bali wangekinukuu kifungu kwa kubalansi ili kuitunza maana halisi ya mwandishi, lakini bila kufanya hivyo shuhuda zitatumika katika njia ya kupotosha na kujeruhi nafsi za watu. Ellen White anaendelea kukemea swala hili:

"Kutakuwa na wale ambao watatafisiri vibaya na kuwakilisha vibaya. Macho yao yamepofushwa, na wanaweka mifano na tafisiri ambazo Shetani amefanya kazi kwa ajili yao, na maana ya kosa kabisa itawekwa juu ya maneno ambayo Dada White ameyasema. Shetani anadai kabisa kuwa mtoto wa Kristo kama alivyofanya Yuda, ambaye alikuwa upande wa shutuma. Wamejifundisha wao wenyewe katika shule ya Shetani ya kuelezea vibaya." —(Ellen G. White, Sellected Messages Book 1, p. 57, par. 3); pia The Writing and Sending Out of the Testimonies to the Church, p. 25a .2; na Manuscript 23, October 10, 1911, par. 2)))

"Na wakati ninapokutana na ushahidi kwamba mawasiliano hayo yatashughulikiwa na baadhi kwa mujibu wa hukumu ya kibinadamu ya wale watakaozipokea; wakati ninapotambua kwamba baadhi wanaangalia kwa bidii kwa ajili ya baadhi ya maneno ambayo yametokana na kalamu yangu na ambayo juu yake wanaweza kuweka utafsiri wao wa kibinadamu ili kuendeleza nafasi zao na kuhalalisha mwenendo mbaya wa hatua—wakati ninapofikiria mambo haya, haitii moyo sana kuendelea kuandika. Baadhi ya wale ambao kwa hakika wamekemewa wanajitahidi kufanya kila neno kuitetea kauli yao wenyewe. Mitikisiko na hila na utafsiri mbaya na matumizi mabaya ya Neno ni vya ajabu. Watu wamehusishwa pamoja katika kazi hii. Kile ambacho mmoja hakifikirii, akili nyingine inakisambaza." —(Ellen G. White, Letter (Lt) 172, June 14, 1906, par. 4); pia Sellected Message Book 3, pp. 81,82; Manuscript Releases, vol. 4, p. 64.2; na The Paulson Collection, p. 33.3)))


This website was built using N.nu - try it yourself for free.    (Click here to renew the premium)